Jumanne, 19 Januari 2016

Ngeli za nomino za kiswahili




SWALI: Kwa kutumia mifano, ainisha ngeli za nomino za Kiswahili, kwa kigezo cha kimofolojia. Kisha jadili upungufu wa uainishaji huo.
                                               
                                                               
Fasili ya ngeli imejadiliwa na wataalamu na wanazuoni mbalimbali, huku kila mtaalamu akiwa na mtazamo wake juu ya dhana hii. Baadhi ya wataalamu na wanazuoni hao ni kama hawa wafuatayo:
Mgullu (1999: 148) anasema istilahi “ngeli” imechukuliwa kutoka lugha ya Kihaya (Tanzania). Katika lugha ya kihaya neno “ngeli” lina maana ya aina ya kitu. 

Mgullu (1999: 148) akiinukuu Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981) anaeleza kuwa ngeli ni utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za majina (nomimo) kama vile ki-vi, ma, n.k.
Mgullu anaendelea kusema kuwa fasili hii inapotosha. Tuaamini ya kuwa ngeli ni kundi la nomino za aina moja na si ule utaratibu wa kupanga nomino katika makundi kama fasili ya hapo juu inavyodai.
TUKI (1990) wanaeleza kuwa ngeli za nomino ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi vinavyofanana. Fasili hii inaonekana ni bora lakini tatizo lake ni kuwa imeweka pamoja vigezo viwili, yaani kigezo cha kisintaksia na kile cha kimofolojia. Kwa maoni yangu ni kuwa vigezo hivi haviwezi kutumika pamoja kwa sababu havina uhusiano wa moja kwa moja. Wanaisimu na wachambuzi wengi wa awali walijaribu kuvitumia vigezo vyote viwili kwa pamoja wakati wa kuainisha ngeli za nomino za Kiswahili lakini walishindwa. Hali hii imesababisha uainishaji wa ngeli katika lugha ya Kiswahili uonekane kuwa wa kutatanisha.

Massamba, D.P.B na Wenzake (2012) wanasema kauli kwamba ngeli ni mgawanyiko wa aina mbalimbali za nomino katika mtazamo wa kisarufi katika fikra ya viashirio vya nomino katika aina nyingine za maneno zinazoandamana nazo. Kwa maelezo mafupi tunaweza kusema ngeli za nomino huhusu makundi ya majina; kila kundi likiwa na mabadiliko ya aina moja ya viambishi vya umoja na wingi vyenye kuleta upatanishi wa kisarufi wa namna moja katika vitenzi, vivumishi na viwakilishi. Kila ngeli ina kiambishi cha nomino zake ambacho kinatawala viambishi vinavyorejea nomino hiyo katika aina hizo nyingine ziandamanazo nayo.

Massamba na Wenzake wanaendelea kufafanua kuwa kila lugha inayotumia utaratibu wa ngeli huwa ina idadi fulani ya ngeli. Si rahisi kusema kwa yakini hapo zamani lugha za kibantu zilikuwa na ngeli ngapi, lakini tunajua kwamba kwa wastani lugha nyingi zina ngeli zisizopungua kumi na zisizozidi ishirini. 

Kwa ujumla, ngeli ni aina au namna ya kupanga au kuweka majina katika makundi yanayofanana au yanayowiana. Majina ya Kiswahili yanaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali. Baadhi ya wanaisimu wamegawanya majina katika makundi 16 na wengine katika makundi 9 na wengine makundi 18. Wanaisimu tofauti walioainisha ngeli za majina ya Kiswahili wamechunguza vipengele tofauti  vya majina na kuyaanisha tofauti. Nomino za lugha fulani zinaweza kuainishwa kwa kutumia vigezo vikuu vitatu yaani:
·        
            Kigezo cha kisematiki
·         Kigezo cha kimofolojia
·         Kigezo cha kisintaksia

Lakini katika muktadha huu tutajikita katika kujadili uainishaji wa ngeli za Kiswahili kwa kutumia kigezo cha kimofolojia. Kigezo cha kimofolojia ni kigezo kikongwe zaidi kilichotumiwa na wanasarufi mapokeo, miongoni mwao akiwa Meinhof ambao waliyaainisha kulingana na maumbo ya viambishi awali vya majina. Majina yote yalikuwa na viambishi awali vinavyofanana yaliwekwa katika kundi moja na kufanya ngeli moja kutokana na kigezo hiki kuna ngeli 18 za Kiswahili. Uainishaji wao ni kama ifuatavyo:
Ngeli
Mfano wa majina ya Ngeli
1-Mu-
2-Wa-
Mzee – wazee
Mtoto- watoto
3- M-
4- Mi-
Mti – miti
Mchungwa – michungwa
5- Ki-
6- Vi-
Kiti- viti
Kisu- visu
7- Ji-
8- Ma-
Jiwe- mawe
Jicho- macho
9- N-
10.
Nguo, nchi, njaa, nyota, ngozi, nyama
11- U-
12- N-
Uso – nyuso
Uzi – nyuzi
Ulimi- ndimi
13- U-
14- Ma-
Uasi – maasi
Ugonjwa – magonjwa
15- Ku-
Kusoma
Kucheza
Kuimba
Kuruka
16- Pa-
Pahali
17- Mu-
Muhali
18- Ku-
Kuhali

Wanaisimu wengine Ashtoni (1944) na Broomfield (1930) waliainisha majina baada ya Meinhof, walifuatisha mtindo wa Meinhof, isipokuwa wanayaweka katika ngeli moja majina ya umoja na uwingi ambayo yanachangia mzizi mmoja badala ya kuyaona kuwa ni tofauti. Kwa uainishaji huu walipunguza idadi ya ngeli  hadi kufikia 9 tu.
Ngeli
Mifano ya Majina
1-Mu/Wa
Mtoto – watoto
Mpishi – wapishi
Mchungaji – wachungaji
Mkulima – wakulima
Mtu – watu
2- M/Mi
Mti – miti
Mwembe – miembe
Mkono – mikono
Mchoro – michoro
3- Ki/Vi
Kiti – viti
Kitabu- vitabu
Kito-vito
Kisu-visu
4- N
Ngozi, nyota, nyundo, njia, ngoma, njuga
5- Ji/Ma
Jiwe – mawe
Jino – meno
6- U/N
Uzi – nyuzi
Uso – nyuso
Ulimi – ndimi
Ufa – nyufa
7-U/Ma
Ugonjwa – magonjwa
Uasi – maasi
Ununuzi – manunuzi
8- Ku

Kuimba, kucheza, kuoga, kupiga, kusoma, kuruka, kulima

9- KU
    PA
    Mu
Mahali Kule
            Pale
            Mule

Uainishaji wa akina Ashton na Broomfield unafanana na ule wa Meinfoh kwa sababu wote wameegemea uainishaji wao katika umbo la viambishi awali vya majina. Hata hivyo uainishaji wao umekuwa mwepesi zaidi kwa mtu anayejifunza ngeli za majina kwa vile unaonesha uhusiano wa umbo la umoja na uwingi la majina ya aina moja. Zaidi ya hayo uchache wa ngeli hizi unamfanya mwanafunzi azikumbuke kwa urahisi.

Matatizo (Mapungufu) ya kigezo hiki
-          Kuna viambishi ambavyo vinafanana, mfano, ngeli ya kwanza inawakilishwa na kiambishi Mu, kiambishi hiki kinajitokeza vilevile katika ngeli ya pili na ngeli ya tisa. Hali kadhalika vile vya ngeli ya nne na sita vinawakilishwa na kiambishi N-, ngeli za sita na saba inawakilishwa na kiambishi U-. kwa ujumla hili ni tatizo.
-          Kuna majina mengine hayana umbo dhahiri la umoja na uwingi mfano tunda, nguo. Hivyo inakuwa vigumu kuainisha majina yasiyo na umbo dhahiri la umoja na uwingi kwa kutumia kigezo hiki.  
-          Pia kigezo hiki kinachanganya majina ya viumbe hai na visivyo viumbe hai mfano ngeli ya tatu Ki – Vi                                                                                                                                                              umoja           uwingi                                                                                                                              kiti                 viti   (kiumbe kisicho na uhai)                                                                                      kijana               vijana (kiumbe hai) 
-          Kuna baadhi ya ngeli zina viambishi vya umoja tu mfano ngeli ya nne inatumia kiambishi cha umoja N- .
-          Pia kigezo hiki hakitilii maanani muundo wa sentensi.

Mgullu (1999: 156) naye amejaribu kuainisha kwa kutumia kigezo hiki cha kimofolojia. Mgullu katika kuhitimisha uainishaji wake anasema kuwa ngeli nomino za kimofolojia katika lugha ya Kiswahili zipo tisa yaani ngeli za:
          i.            MU-WA
        ii.            M-MI
      iii.            JI-MA
      iv.            KI-VI
        v.            U-N
      vi.            U-MA
    vii.            U-ϴ
  viii.            ϴ-MA
      ix.            ZISIZO NA KIAMBISHI (CHA IDADI) CHOCHOTE

Mgullu anaendelea kufafanua kuwa katika uainishaji huu utagundua ya kuwa nomino zilizo na umoja na wingi tumeweziweka katika kundi moja tu. Utaona ya kuwa uainishaji huu unatuwezesha kuzigawa nomino zote za Kiswahili bila kuibakisha hata nomino moja. Unaweza kufikiria nomino yoyote na utapata mahali muafaka unapoweza kuiweka.                                               

    Dosari za uainishaji wa Mgullu ni kuwa bado matatizo tulioyataja hapo juu kwa wataalamu na wanaisimu wengine bado hata kwa Mgullu yamejitokeza sana mfano kufanana kwa viambishi, baadhi ya ngeli hazina umoja na wingi, pia amechanganya majina ya viumbe hai na visivyo hai na katika uainishaji wa Mgullu hatujaona ngeli ya PA-MU-KU.

Hitimisho                                                                                                                                             Kwa kuwa tumeshaona mapungufu na matatizo ya uainishaji wa wataalamu na wanaisimu hao, kuna haja ya wanaisimu na wanazuoni kuendelea kufanya utafiti na uchunguzi ili kuondoa haya mapungufu.



                                            VITABU VYA REJEA   
Massamba, D.P.B. na Wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA) Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TUKI.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.

Rubanza, Y.I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Tanzania.

Taasisi ya Elimu (1996). Kiswahili Kidato 1-4. Dar es Salaam: Oxford University Press.

TUKI. (1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI.

Swalo, D.B. (Muswada). Darasa la Kiswahili: Kidato cha Tano na Sita

Maoni 1 :