Jumamosi, 3 Mei 2014

NADHARIA KUHUSU CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI

  1. NADHARIA KUHUSU CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI

Chanzo na Chimbuko la fasihi simulizi                                                                                            Wataalamu wa fasihi simulizi, wamezuka na nadharia kadha kuelezea asili, chanzo, chimbuko, ukuaji na ueneaji wa fasihi simulizi. Kuna nadharia kuu tatu zinaelezea kuhusu chimbuko na chanzo cha fasihi simulizi, ambazo ni:
1.      Nadharia ya kiulimwengu (utandawazi), imegawanyika katika sehemu tatu, ambazo ni:   - Ubadilikaji
- Msambao
- kisosholojia
2.      Nadharia ya utaifa
3.      Nadharia ya hurutishi

1. Nadharia ya Kiulimwengu (Utandawazi)                                                                                     Hii ndiyo nadharia ya kwanza kuelezea kuhusu chimbuko na chanzo cha fasihi simulizi. Watafiti wa nadharia hii walikuwa wazungu wa Ulaya, hivyo nadharia hii iliegemea zaidi mtazamo wa Kimagharibi. Mawazo ya nadharia ya kiulimwengu yamegawanyika katika makundi matatu:
(a) Ubadilikaji Taratibu                                                                                                                            Muasisi wa nadharia hii ni Charles Dawin (1809-1882), na wafuasi wake waliamini kuwa kuna misingi anuai kuhusu kanuni zinazoongoza asili na maendeleo ya utamaduni wa mwanadamu. Kundi hili liliona kuwa dhana ya ubadilikaji taratibu misingi yake mikuu ni viumbe hai. Wanasema viumbe hai vyote vinakuwa katika mchakato wa mabadiliko mbalimbali hadi kufikia kwenye maumbo yao ya sasa. Hivyo na fasihi simulizi imepitia michakato mingi ya mabadiliko mpaka kufikia katika umbo lake la sasa, mfano fasihi simulizi ya kipindi cha Ujima ni tofauti na fasihi iliyofuata katika vipindi vingine kama vile wakati wa Utumwa, Ubepari hata mfumo tulionao sasa.                                                                                                                            Hivyo, fasihi similizi ya kiafrika hubadilika kutoka kipindi kimoja hata kingine kutokana na mabadiliko ya kijamii. Kwa ujumla waasisi hawa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni jamii yenyewe na kutokea kwa kufanana kwa kazi za fasihi simulizi kutoka jamii moja hadi nyingine kunasababishwa na hatua sawa za mabadiliko kiakili na kijamii kwani jamii moja iliyozagaa ulimwenguni kote akili zao ni sawa.                                                                                                                           
Dosari ya nadharia hii ni kwamba waliziona kazi za fasihi simulizi za Kiafrika kwamba hazina mwenyewe kwa kuwa ni mali ya jamii nzima. Walisema kwamba, ijapokuwa fasihi simulizi ni mali ya jamii, lakini sio kwa kiwango hicho walichokisema wao. Walisisitiza kuwa si kila mzungumzaji anaweza kuwa fanani wa fasihi simulizi. Wao walilipuuza suala la upekee wa muktadha.

Ubora wa nadharia ya kiulimwengu (kitandawazi)          
Ø  Mchango wao katika nadharia ya fasihi simulizi, umechangia kuibuka kwa nadharia nyingine zinazoeleza kuhusu chanzo na chimbuko la fasihi simulizi.
Ø  Wanakubali kwamba Afrika ilikuwa na fasihi simulizi.
Ø  Waliweza kubaini baadhi ya tanzu za fasihi simulizi, mfano hadithi za kale, methali, vitendawili, jado na unyago, kusalia miungu, mivigha, n.k.

Udhaifu wa nadharia hii
Ø  Mtazamo huu ulikuwa wa kimagharibi zaidi, hivyo,waliegemea zaidi utamaduni wa Ulaya.
Ø  Walijikita zaidi kuelezea historia ya utamaduni wa Kiafrika na kusahau kutafiti kazi za fasihi simulizi.
Ø  Nadharia zao zilikuwa za kufikirika zaidi, hivyo ni vigumu kuzithibitisha kisayansi.
Ø  Walisisitiza zaidi mfanano kana kwamba jamii hizi hazikuwa hazina tofauti yoyote katika kazi zao.

(b) Msambao                                                                                                                                      Waasisi wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na wanaubadilikaji taratibu ambao (wanaubadilikaji taratibu) waliamini kuwa kufanana kwa fani mbili za kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa za kimaendeleo, wanamsambao  wanaamini kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea sababu ya msingi ya mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani jamii hizo ziliwahi kukutana kwa namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana baadhi ya mila na desturi.                   Kwa ujumla mawazo ya wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa kutoka katika jamii imara, yenye nasabu bora, jamii iliyostaarabika na maarufu tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo dhaifu au duni. Hivyo basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi ya kiafrika ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda sehemu nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano, ushairi wa simulizi wa kiswahili ulitoka Uarabuni na Uajemi kuja Afrika na huko ndiko ambako kulionekana kuwa kumestaarabika kuliko Afrika na ndiyo maana ushairi huo uliletwa huku Afrika.                                                                                                                                            
 Dosari ni kwamba, wananadharia hii wanaamini kuwa chimbuko na asili ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni Ulaya, jambo ambalo hatuwezi kukubaliana nalo kwani kila jamii ina fasihi yake na kutokea mfanano wa baadhi ya kazi za fasihi huenda kuna kuathiriana kwa namna fulani miongoni mwa jamii hizo.                                                                                                                              
 Dosari nyingine ni kwamba, si kweli kuwa jamii duni, isiyostaarabika au zinazoendelea hazina fasihi yoyote, kama walivyodai wana nadharia hii. Upo ushahidi unaothibitisha kwamba lugha za Kiulaya na fasihi yake zimeiga (zimeathiriwa) mambo ya Kiafrika, kwa mfano, neno shamba, ugali, mama katika Kiingereza ni wazi yametoka katika lugha za Kiafrika, hususan Kiswahili; pia uchezaji wa kukata viuno Ulaya si asili yao, hasa ni utamaduni wa Kiafrika, mavazi ya khanga na kadhalika. Aidha hawatoi ushaidi wa kisayansi wa uduni wa bara la Afrika.                                  
 Pia, wanamsambao walisisitiza zaidi ufanano na kupuuza tofauti. Kwao walieleza ufanano kana kwamba jamii hazikuwa na tofauti yoyote katika kazi hizo za fasihi. Kwa kuwa jamii hizi ziliishi katika mazingira tofauti na zilikuwa na kiwango tofauti cha maendeleo, ilikuwa wazi kwamba kulikuwa na tofauti pia.

(c) Nadharia ya Kisosholojia                                                                                                          Sosholojia ni taaluma inayochunguza mfumo wa kijamii, yaani mahusiano ya wanajamii, mfumo wa kiutawala wa kijamii, maendeleo ya kijamii na kadhalika. Baada ya kugundua kuwa nadharia ya ubadilikaji taratibu na msambao zina mapungufu, ndipo nadharia hii ikaibuka. Nadharia hii ya kisosholojia ina mihimili mitatu ambayo ni ule wa Umahususi na sio umajumui, mkazo katika utendaji na mhimili unaosisitiza dhima ya fasihi simulizi katika jamii.
\
Umahususi
Kwa kuanza na mhimili wa Umahususi, nadharia hii ilijikita zaidi katika jamii peke yake badala ya kujikita katika taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla kama walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi. Hii ilikuwa baada ya kugundua dosari zilizofanywa hapo kabla, Dosari ya kutoa tamko la juu juu na la jumla zaidi ambapo matamko hayo mara nyingi yalitupilia mbali vipengele fulani vya lugha na mienendo mingine ya jamii.

Mhimili wa utendaji
Pia katika mhimili wa utendaji, Wanasosholijia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji (performance) wa kazi mbalimbali ya fasihi simulizi. Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya fasihi wanaujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa husika na jambo hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha utendaji. Vilevile  wamedokeza sifa za ndani za fasihi simulizi ya kiafrika, na hivyo wao wanaona kuwa ili kujua fasihi simulizi ya kiafrika ni vyema kuangalia jamii na utendaji wa kazi husika.

 Dhima ya fasihi simulizi katika jamii
 Katika msisitizo juu ya dhima ya fasihi simulizi katika jamii, Wanasosholojia wanaamini kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.
Hivyo ili kuelewa historia ya fasihi simulizi kutokana na mawazo ya wanasosholojia ni wazi kwamba unapaswa kuangalia jamii husika, utendaji na dhima ya fasihi katika jamii husika, kwani mihimili hii ndiyo chanzo au historia ya fasihi simulizi ya jamii husika. kutokana na mawazo ya wananadharia hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya kiafrika ni ndani ya jamii za Kiafrika zenyewe na si vinginevyo.                                                                                                               Dosari ya nadharia hii ni kwamba ingawa walijitahidi kuipa hadhi kwa kusisitiza upekee wa muktadha wa kijamii wa fasihi simulizi ya Kiafrika tofauti na waliotangulia hawakuchunguza kwa undani sifa za kisanaa za fasihi simulizi. Wameandika ngano kwa namna ya kupwaya, hazivutii. Wameshindwa kuchambua sanaa kubwa iliyomo kwenye matini chanzi nyingi za kifasihi simulizi walizochunguza (uradidi, mishtuko, wombo, n.k.). Hivyo basi, haikuwa rahisi kuuona ufasihi kwa ujumla wake kutokana na tafiti za kisosholojia kwasababu fasihi ni sanaa na hubebwa na fani na maudhui.   

2.NadhariayaUtaifa                                                                                                                                     
Nadharia hii ilizuka kwenye vugu vugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa  wanadai kuwa wananadharia wa nadharia ya ulimwengu hawakuwa  na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za kiafrika, Kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na wazungu kupita mlango wa ukoloni.
                Nadharia ya Utaifa, imeasisiwa na S. Adeboye, Babalola, Daniel P. Kunene na J. P Clark. Katika nadharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa kuondoa. Kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti bali kuyahariri matokeo yao. Na wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.                                               
 Hivyo ili kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu na wanazuoni wa taifa au jamii hiyo. Kwasababu wataalamu na wanazuoni hao ndiyo wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.                                                              
  Kiujumla wananadharia ya kitaifa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ya kiafrika inapatikana ndani na jamii ya kiafrika na ili kuchunguza fasihi ya jamii husika sharti wataalamu na wanazuoni wa jamii hiyo wahusishwe.

3. Nadharia ya Hulutishi                                                                                                              Nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni wa kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza taaluma ya fasihi ya kiafrika. Wananadharia hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni na ya kijadi zimeathiriana na kuingiliana. Miongoni mwa waasisi na watetezi wa nadharia hii ni pamoja na M.M. Mulokozi, Johnson, Ngugi wa Thiong`o, Chinua Achebe, Frantz Fanon, Abiola Irele, Taban Lo Liyong, n.k.  Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na wakijadi.                                                                                                                                     
 Wao walianza kuandika kazi za fasihi ambazo zinajaribu kuhusianisha ujadi wa Waafrika na usasa unaotokana na ujio wa wageni. Kwa mfano, Chinua Achebe katika Things Fall Apart, No Longer At Ease; Ngugi wa Thiongʼo katika The Grain of Wheat na Lo Liyong, T. (1972), Popular Culture of East Africa, Nairobi: (Longman Kenya) n.k. mtazamo huu umekuwa maarufu na kwa kiasi kikubwa bado unatumika. Hata utafiti wa Samwel unajaribu kuangalia ujadi wa majigambo na usasa.       
Hitimisho                                                                                                                                              Kwa ujumla nadharia zote tatu zimejaribu kuangalia chimbuko la fasihi simulizi na kutoa muelekeo kuhusu asili ya fasihi simulizi ya kiafrika. Kazi za fasihi zimeanza tangu binadamu walipoanza kuishi pamoja. Kazi hizo zilisimuliwa na kuaksi shughuli zilizokuwa zinafanywa na watu katika mazingira ya wakati huo. Kadri mazingira yalivyobadilika, hali kadhalika mambo yaliyosimuliwa yalibadilika. Kwa mfano, watu waliokuwa wanalima viazi, masimulizi yao yalihusiana na kilimo na matumizi ya viazi. Lakini baadaye watu hawa waliletewa mfumo wa kulima pamba. Kwa hiyo, masimulizi yao yalibadilika na kuelekea kwenye kilimo na matumizi ya pamba.                                                                                                                                                         
Vile vile waliotumia pinde na mishale katika uwindaji waliunda masimulizi yahusuyo maumbo na matumizi ya vifaa hivyo. Jamii hiyo ikipata na kutumia bunduki itabidi misemo na masimulizi yanayohusiana na bunduki.                                                                                                  
 Kwa hiyo fasihi simulizi ya kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni lakini ilianza kupata athari mara baada ya ujio wa wageni, athari na muingiliano wa fasihi simulizi hauoneshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwakuwa fasihi yoyote lazima iathiriwe na iathiri fasihi nyingine. Hivyo basi, kila jamii au taifa huwa na fasihi yake na utamaduni wake ambapo maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza kuathiriana na hivyo kuathiri pia fasihi ya jamii husika.

Maoni 24 :

  1. kazi nzuri. Heko!.. Maseno, Kenya

    JibuFuta
  2. asante Kinyanjui Ngigi kutoka Kenya

    JibuFuta
  3. Safi kabisa.mmenisaidiaIngiza maoni yako...

    JibuFuta
  4. ahsanteni sana tunaomba na nadharia ya fasihi kwa ujumla

    JibuFuta
  5. Kazi nzuri,ila tu nakukumbusha kuwa katika kushadidia hoja yako ya nadharia ya msambao,umezungumzia fasihi na uchezji wa kukata viuno,nukukumbusha atu fasihi uti wake wa mgongo/pumzi yake ni lugha.

    JibuFuta
  6. Fasihi ya kimagharibi ni sawa Na fasihi ya kimajaribio naombeni majibu

    JibuFuta
  7. Aksante nimeongeza uelewa mola akupe wepesi

    JibuFuta
  8. Asante kwa kaz mzuri ila nlitaka kujua je kuna udhaifu wowote katika nadharia ya utaifa had ikatokea nadharia ya uhulutishi?

    JibuFuta
  9. Ahsante sana kwa hiki mlichokitoa kwa ajili kusaidia kuinua maarifa ya watu hasa wanafunzi✍🙏🙏

    JibuFuta
  10. Kazi ni nzuri tunaomba marejeleo

    JibuFuta
  11. Jibu.jadili nafasi ya nadharia ya kiasili ukirejelea riwaya ulosoma

    JibuFuta
  12. Kazi nzuri ila ni dhaifu kwani imekosa marejeleo

    JibuFuta
  13. Fasihi simulizi iko vizuri

    JibuFuta
  14. Vipi kuhusu uhisiano uliokuwepo Kati ya fasihi simulizi wakati wa ujima na jamii za wakati huo

    JibuFuta
  15. kaz nzuri..ila nauliza kuna tofauti yoyote kati ya nadharia moja na nyingine!

    JibuFuta
  16. Kazi nzuri vipi kuna mchango wowote wa nadharia ya utaifa ilivyosaidia kuchakata data

    JibuFuta
  17. Kazi zuri sana mwanafasihi simulizi

    JibuFuta
  18. Nataka kujua tofauti iliyopo kati ya fasihi ya kipindi cha utumwa na kipindi hiki cha utandawazi

    JibuFuta
  19. Kazi nzuri lake marejeleo

    JibuFuta