- NADHARIA KUHUSU CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI
Chanzo na Chimbuko la
fasihi simulizi
Wataalamu wa fasihi
simulizi, wamezuka na nadharia kadha kuelezea asili, chanzo, chimbuko, ukuaji
na ueneaji wa fasihi simulizi. Kuna nadharia kuu tatu zinaelezea kuhusu
chimbuko na chanzo cha fasihi simulizi, ambazo ni:
1. Nadharia ya kiulimwengu (utandawazi),
imegawanyika katika sehemu tatu, ambazo ni:
- Ubadilikaji
-
Msambao
-
kisosholojia
2. Nadharia ya utaifa
3. Nadharia ya hurutishi
1. Nadharia ya
Kiulimwengu (Utandawazi)
Hii ndiyo nadharia
ya kwanza kuelezea kuhusu chimbuko na chanzo cha fasihi simulizi. Watafiti wa
nadharia hii walikuwa wazungu wa Ulaya, hivyo nadharia hii iliegemea zaidi
mtazamo wa Kimagharibi. Mawazo ya nadharia ya kiulimwengu yamegawanyika katika
makundi matatu:
(a) Ubadilikaji
Taratibu Muasisi wa
nadharia hii ni Charles Dawin (1809-1882), na wafuasi wake waliamini kuwa kuna
misingi anuai kuhusu kanuni zinazoongoza asili na maendeleo ya utamaduni wa
mwanadamu. Kundi hili liliona kuwa dhana ya ubadilikaji taratibu misingi yake
mikuu ni viumbe hai. Wanasema viumbe hai vyote vinakuwa katika mchakato wa
mabadiliko mbalimbali hadi kufikia kwenye maumbo yao ya sasa. Hivyo na fasihi
simulizi imepitia michakato mingi ya mabadiliko mpaka kufikia katika umbo lake
la sasa, mfano fasihi simulizi ya kipindi cha Ujima ni tofauti na fasihi
iliyofuata katika vipindi vingine kama vile wakati wa Utumwa, Ubepari hata
mfumo tulionao sasa. Hivyo, fasihi similizi ya kiafrika hubadilika kutoka kipindi kimoja hata
kingine kutokana na mabadiliko ya kijamii. Kwa ujumla waasisi hawa wanaamini
kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni jamii yenyewe na kutokea kwa kufanana kwa
kazi za fasihi simulizi kutoka jamii moja hadi nyingine kunasababishwa na hatua
sawa za mabadiliko kiakili na kijamii kwani jamii moja iliyozagaa ulimwenguni
kote akili zao ni sawa.
Dosari
ya nadharia hii ni kwamba waliziona kazi za fasihi simulizi za Kiafrika kwamba hazina mwenyewe kwa
kuwa ni mali ya jamii nzima. Walisema kwamba, ijapokuwa fasihi simulizi ni mali
ya jamii, lakini sio kwa kiwango hicho walichokisema wao. Walisisitiza kuwa si
kila mzungumzaji anaweza kuwa fanani wa fasihi simulizi. Wao walilipuuza suala
la upekee wa muktadha.
Ubora wa nadharia ya kiulimwengu
(kitandawazi)
Ø Mchango wao
katika nadharia ya fasihi simulizi, umechangia kuibuka kwa nadharia nyingine
zinazoeleza kuhusu chanzo na chimbuko la fasihi simulizi.
Ø Wanakubali kwamba
Afrika ilikuwa na fasihi simulizi.
Ø Waliweza kubaini
baadhi ya tanzu za fasihi simulizi, mfano hadithi za kale, methali,
vitendawili, jado na unyago, kusalia miungu, mivigha, n.k.
Udhaifu wa nadharia hii
Ø Mtazamo huu
ulikuwa wa kimagharibi zaidi, hivyo,waliegemea zaidi utamaduni wa Ulaya.
Ø Walijikita zaidi
kuelezea historia ya utamaduni wa Kiafrika na kusahau kutafiti kazi za fasihi
simulizi.
Ø Nadharia zao zilikuwa
za kufikirika zaidi, hivyo ni vigumu kuzithibitisha kisayansi.
Ø Walisisitiza
zaidi mfanano kana kwamba jamii hizi hazikuwa hazina tofauti yoyote katika kazi
zao.
(b) Msambao
Waasisi
wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na
wanaubadilikaji taratibu ambao (wanaubadilikaji taratibu) waliamini kuwa
kufanana kwa fani mbili za kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa
za kimaendeleo, wanamsambao wanaamini
kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea sababu ya msingi ya mfanano
huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani jamii hizo ziliwahi kukutana kwa
namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana baadhi ya mila na
desturi. Kwa ujumla
mawazo ya wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa
kutoka katika jamii imara, yenye nasabu bora, jamii iliyostaarabika na maarufu
tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo dhaifu au duni. Hivyo
basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi ya kiafrika
ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda sehemu
nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano, ushairi wa simulizi wa
kiswahili ulitoka Uarabuni na Uajemi kuja Afrika na huko ndiko ambako
kulionekana kuwa kumestaarabika kuliko Afrika na ndiyo maana ushairi huo
uliletwa huku Afrika.
Dosari ni kwamba, wananadharia
hii wanaamini kuwa chimbuko na asili ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni Ulaya,
jambo ambalo hatuwezi kukubaliana nalo kwani kila jamii ina fasihi yake na
kutokea mfanano wa baadhi ya kazi za fasihi huenda kuna kuathiriana kwa namna fulani
miongoni mwa jamii hizo.
Dosari
nyingine ni kwamba, si kweli kuwa jamii duni, isiyostaarabika au zinazoendelea
hazina fasihi yoyote, kama walivyodai wana nadharia hii. Upo ushahidi
unaothibitisha kwamba lugha za Kiulaya na fasihi yake zimeiga (zimeathiriwa)
mambo ya Kiafrika, kwa mfano, neno shamba, ugali, mama katika Kiingereza ni
wazi yametoka katika lugha za Kiafrika, hususan Kiswahili; pia uchezaji wa kukata
viuno Ulaya si asili yao, hasa ni utamaduni wa Kiafrika, mavazi ya khanga na
kadhalika. Aidha hawatoi ushaidi wa kisayansi wa uduni wa bara la Afrika.
Pia,
wanamsambao walisisitiza zaidi ufanano na kupuuza tofauti. Kwao walieleza
ufanano kana kwamba jamii hazikuwa na tofauti yoyote katika kazi hizo za
fasihi. Kwa kuwa jamii hizi ziliishi katika mazingira tofauti na zilikuwa na
kiwango tofauti cha maendeleo, ilikuwa wazi kwamba kulikuwa na tofauti pia.
(c)
Nadharia ya Kisosholojia Sosholojia ni taaluma inayochunguza
mfumo wa kijamii, yaani mahusiano ya wanajamii, mfumo wa kiutawala wa kijamii,
maendeleo ya kijamii na kadhalika. Baada ya kugundua kuwa nadharia ya
ubadilikaji taratibu na msambao zina mapungufu, ndipo nadharia hii ikaibuka. Nadharia
hii ya kisosholojia ina mihimili mitatu ambayo ni ule wa Umahususi na sio umajumui, mkazo
katika utendaji na mhimili unaosisitiza dhima
ya fasihi simulizi katika jamii.
\
Umahususi
Kwa
kuanza na mhimili wa Umahususi, nadharia hii ilijikita zaidi katika
jamii peke yake badala ya kujikita katika taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla kama
walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi. Hii ilikuwa baada ya
kugundua dosari zilizofanywa hapo kabla, Dosari ya kutoa tamko la juu juu na la
jumla zaidi ambapo matamko hayo mara nyingi yalitupilia mbali vipengele fulani
vya lugha na mienendo mingine ya jamii.
Mhimili
wa utendaji
Pia
katika mhimili wa utendaji, Wanasosholijia
waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji (performance) wa kazi mbalimbali
ya fasihi simulizi. Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya
fasihi wanaujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa husika na jambo hili
limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha utendaji.
Vilevile wamedokeza sifa za ndani za
fasihi simulizi ya kiafrika, na hivyo wao wanaona kuwa ili kujua fasihi
simulizi ya kiafrika ni vyema kuangalia jamii na utendaji wa kazi husika.
Dhima ya fasihi simulizi katika jamii
Katika msisitizo juu ya dhima ya fasihi simulizi katika jamii, Wanasosholojia
wanaamini kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba
unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.
Hivyo ili kuelewa historia ya fasihi simulizi
kutokana na mawazo ya wanasosholojia ni wazi kwamba unapaswa kuangalia jamii
husika, utendaji na dhima ya fasihi katika jamii husika, kwani mihimili hii
ndiyo chanzo au historia ya fasihi simulizi ya jamii husika. kutokana na mawazo
ya wananadharia hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya kiafrika ni ndani
ya jamii za Kiafrika zenyewe na si vinginevyo. Dosari ya
nadharia hii ni kwamba ingawa walijitahidi kuipa hadhi kwa kusisitiza upekee wa
muktadha wa kijamii wa fasihi simulizi ya Kiafrika tofauti na waliotangulia
hawakuchunguza kwa undani sifa za kisanaa za fasihi simulizi. Wameandika ngano
kwa namna ya kupwaya, hazivutii. Wameshindwa kuchambua sanaa kubwa iliyomo
kwenye matini chanzi nyingi za kifasihi simulizi walizochunguza (uradidi,
mishtuko, wombo, n.k.). Hivyo basi, haikuwa rahisi kuuona ufasihi kwa ujumla
wake kutokana na tafiti za kisosholojia kwasababu fasihi ni sanaa na hubebwa na
fani na maudhui.
2.NadhariayaUtaifa
Nadharia
hii ilizuka kwenye vugu vugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa wanadai kuwa wananadharia wa nadharia ya
ulimwengu hawakuwa na uelewa wa kutosha
kuhusu lugha za kiafrika, Kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni
na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa
na aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na wazungu kupita
mlango wa ukoloni.
Nadharia ya
Utaifa, imeasisiwa na S. Adeboye, Babalola, Daniel P. Kunene na J. P Clark.
Katika nadharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita
zimeshindwa kuondoa. Kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya
kutafiti hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti bali
kuyahariri matokeo yao. Na wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila
kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.
Hivyo ili
kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya kiafrika ni lazima kuhusisha
wataalamu na wanazuoni wa taifa au jamii hiyo. Kwasababu wataalamu na wanazuoni
hao ndiyo wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.
Kiujumla
wananadharia ya kitaifa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ya kiafrika
inapatikana ndani na jamii ya kiafrika na ili kuchunguza fasihi ya jamii husika
sharti wataalamu na wanazuoni wa jamii hiyo wahusishwe.
3. Nadharia ya Hulutishi Nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni
wa kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza
taaluma ya fasihi ya kiafrika. Wananadharia hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni
na ya kijadi zimeathiriana na kuingiliana. Miongoni mwa waasisi na watetezi wa
nadharia hii ni pamoja na M.M. Mulokozi, Johnson, Ngugi wa Thiong`o, Chinua
Achebe, Frantz Fanon, Abiola Irele, Taban Lo Liyong, n.k. Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya
kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu
wote wa kigeni na wakijadi.
Wao
walianza kuandika kazi za fasihi ambazo zinajaribu kuhusianisha ujadi wa
Waafrika na usasa unaotokana na ujio wa wageni. Kwa mfano, Chinua Achebe katika
Things Fall Apart, No Longer At Ease;
Ngugi wa Thiongʼo katika The Grain of Wheat na Lo Liyong, T. (1972), Popular Culture of East Africa, Nairobi: (Longman Kenya) n.k.
mtazamo huu umekuwa maarufu na kwa kiasi kikubwa bado unatumika. Hata utafiti
wa Samwel unajaribu kuangalia ujadi wa majigambo na usasa.
Hitimisho Kwa ujumla nadharia zote tatu
zimejaribu kuangalia chimbuko la fasihi simulizi na kutoa muelekeo kuhusu asili
ya fasihi simulizi ya kiafrika. Kazi za fasihi zimeanza tangu binadamu
walipoanza kuishi pamoja. Kazi hizo zilisimuliwa na kuaksi shughuli zilizokuwa
zinafanywa na watu katika mazingira ya wakati huo. Kadri mazingira
yalivyobadilika, hali kadhalika mambo yaliyosimuliwa yalibadilika. Kwa mfano,
watu waliokuwa wanalima viazi, masimulizi yao yalihusiana na kilimo na matumizi
ya viazi. Lakini baadaye watu hawa waliletewa mfumo wa kulima pamba. Kwa hiyo,
masimulizi yao yalibadilika na kuelekea kwenye kilimo na matumizi ya pamba.
Vile
vile waliotumia pinde na mishale katika uwindaji waliunda masimulizi yahusuyo maumbo
na matumizi ya vifaa hivyo. Jamii hiyo ikipata na kutumia bunduki itabidi
misemo na masimulizi yanayohusiana na bunduki.
Kwa hiyo fasihi simulizi
ya kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni lakini ilianza kupata athari
mara baada ya ujio wa wageni, athari na muingiliano wa fasihi simulizi
hauoneshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwakuwa fasihi yoyote lazima
iathiriwe na iathiri fasihi nyingine. Hivyo basi, kila jamii au taifa huwa na
fasihi yake na utamaduni wake ambapo maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza
kuathiriana na hivyo kuathiri pia fasihi ya jamii husika.
kazi nzuri. Heko!.. Maseno, Kenya
JibuFutaasante Kinyanjui Ngigi kutoka Kenya
JibuFutaSafi kabisa.mmenisaidiaIngiza maoni yako...
JibuFutaahsanteni sana tunaomba na nadharia ya fasihi kwa ujumla
JibuFutaKazi nzuri,ila tu nakukumbusha kuwa katika kushadidia hoja yako ya nadharia ya msambao,umezungumzia fasihi na uchezji wa kukata viuno,nukukumbusha atu fasihi uti wake wa mgongo/pumzi yake ni lugha.
JibuFutaKazi nzuri tu marejeleo hapo?
FutaKazi nzuri sana
JibuFutaFasihi ya kimagharibi ni sawa Na fasihi ya kimajaribio naombeni majibu
JibuFutaAksante nimeongeza uelewa mola akupe wepesi
JibuFutaKaka asante
JibuFutaKazi nzuri
JibuFutaAsante kwa kaz mzuri ila nlitaka kujua je kuna udhaifu wowote katika nadharia ya utaifa had ikatokea nadharia ya uhulutishi?
JibuFutaAhsante sana kwa hiki mlichokitoa kwa ajili kusaidia kuinua maarifa ya watu hasa wanafunzi✍🙏🙏
JibuFutaKazi ni nzuri tunaomba marejeleo
JibuFutaJibu.jadili nafasi ya nadharia ya kiasili ukirejelea riwaya ulosoma
JibuFutaKazi nzuri ila ni dhaifu kwani imekosa marejeleo
JibuFutaFasihi simulizi iko vizuri
JibuFutaVipi kuhusu uhisiano uliokuwepo Kati ya fasihi simulizi wakati wa ujima na jamii za wakati huo
JibuFutakaz nzuri..ila nauliza kuna tofauti yoyote kati ya nadharia moja na nyingine!
JibuFutaKazi nzuri vipi kuna mchango wowote wa nadharia ya utaifa ilivyosaidia kuchakata data
JibuFutaKazi zuri sana mwanafasihi simulizi
JibuFutaNataka kujua tofauti iliyopo kati ya fasihi ya kipindi cha utumwa na kipindi hiki cha utandawazi
JibuFutaKazi nzuri lake marejeleo
JibuFutaKazi mufti. Hongera.
JibuFuta