Jumamosi, 19 Desemba 2015

Fasihi simulizi ya kiswahili na kiafrika



SWALI: Fasihi simulizi ya Kiafrika ni mfumo kamili wa elimu ya maisha ya watu. Kwa kutumia mifano, kutoka fasihi simulizi za jamii mbalimbali za Kitanzania. Jadili rai hii.


Dhana ya fasihi simulizi imeweza kutolewa fasili mbalimbali na wataalamu na wanazuoni mbalimbali, kutoka maeneo tofautitofauti. Fasili hizi mbalimbali zilizotolewa na wanazuoni na wataalamu wengi zimetokana na tofauti miongoni mwao katika mitazamo ya chimbuko la fasihi simulizi, kinadharia na matumizi ya fasihi simulizi kati ya jamii moja na nyingine kumepelekea kuwepo kwa fasili mbalimbali za fasihi simulizi kama ifuatavyo 

Mattelu, M.L., (1983:27) anafafanua kuwa fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumba, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake. Anaendelea kusema kuwa fasihi simulizi ikiwa ni sanaa itumiayo maneno katika kutoa dhana fulani, hutegemea sana nyenzo mbalimbali za kuonekana na kusikika zitumiwazo na binadamu katika kujieleza.                                                                                                                       
Msokile, M (1992:3) fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha, kazi hii ya sanaa huhifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Mwisho anaeleza kuwa fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.                                                            Maelezo haya ya Msokile yanashabihiana na TUKI (2004) fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.                                                                                                          Mazrui na Syambo (1992) wanasema fasihi simulizi ni sanaa ya matumizi ya lugha ya kubuni inayosambazwa kwa mdomo, kwa njia ya kuimba, kuchezwa, kuigizwa, kusimuliwa, kuumba, kufumbua au kutegua mafumbo ya vitendawili.                                                                                Pia naye Mulokozi, M.M (1996) anasema, fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.                                                                                                                                                         Baada ya kuangalia maoni mbalimbali ya wataalamu hao, tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa fasihi simulizi ni aina ya fasihi inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya masimulizi ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi, na hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.                                                                                                                                                         Fasihi simulizi ya Kiafrika ni ile fasihi ambayo kwa asili yake imechimbuka na kuibuliwa na Waafrika wenyewe na huwasilishwa kwa njia ya mdomo kwa kusimuliwa, kuimbwa, kutongolewa au kughaniwa. Fasihi hii ina mawanda mapana kwani hujumuisha jamii zote za Kiafrika na makabila yote ya Kiafrika kama vile Wabuganda kutoka nchini Kenya, Wazulu kutoka Afrika Kusini, Kikuyu kutoka nchini Kenya, Wakinga, Wabena, Wapare, Wasukuma kutoka nchini Tanzania.                                                                                                                             Pia fasihi hii hujumuisha lugha mbalimbali za kiafrika, tamaduni zao, nyimbo zao, mila na desturi zao kama vile matambiko , jando na unyango, kwa mfano kabila la Wakinga linalopatikana mkoani Njombe nchini Tanzania wanamsitu wao ambao watu wa kabila hili huenda kuomba kutatuliwa matatizo yao, shida na shukurani kwa mungu wao, msitu huo unaitwa Nyumba nitu.                                                                                                                                                 Ni kweli kabisa fasihi simulizi ya kiafrika ni mfumo wa elimu ya maisha ya watu. Kauli hii inaweza kufafanuliwa zaidi kwamba, ndani ya fasihi simulizi ambapo kuna tanzu na vipera mbalimbali vinavyotendwa na wasanii katika jamii huchochea na kuhamasisha ujifunzaji, uelewaji na kuongeza maarifa katika mfumo mzima wa maisha ya mtu au jamii. Kupitia vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi kama vile nahau, nyimbo, vitendawili, soga, ngano, tendi, mashairi, majigambo, ngonjera, visasili, na tarihi, vimekuwa kama darasa katika kuleta elimu ya maisha ya watu ndani ya jamii katika kuendesha maisha yao.                                                            Fasihi simulizi huendana na muktadha katika utendaji wake, kama asemavyo Mulokozi, M.M. (1996: 24) kuwa fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha fulani wa jamii na kutawaliwa na mwingiliano wa fanani, hadhira, fani inayotendwa, tukio, mahali na wakati.           
   Hivyo basi, fasihi simulizi ya kiafrika ni mfumo kamili wa elimu ya watu katika muktadha fulani katika jamii fulani, katika shughuli zao za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii kwa sababu zifuatazo:                                                                                                                        
           Kufunza jamii: Fasihi simulizi ya Kiafrika hupelekea mafunzo juu ya maisha ya ndoa. Katika kipengele hiki, vijana waliweza kupata mafunzo ya ndoa kabla ya kuanza maisha ya ndoa. Kwa mfano, Suala la ndoa katika kabila la wasafwa wanaopatikana wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya waliohusika kumfundisha mwali ni shangazi na bibi ambao hasa walikuwa ndio fanani, mwali huyo alifundishwa namna ya kuishi katika ndoa pamoja na matumizi mazuri ya chakula katika familia, kwa mfano binti alifundishwa kupika chakula ambacho kingetosheleza mahitaji ya mumewe na familia yake kwa ujumla bila kubakiza na kukitupa. Katika shughuli hii mwali ndiye aliyekuwa hadhira na ukweni ndio palikuwa mahali pa kutendea na maudhui yalikuwa ni mafunzo kuhusu maisha ya ndoa na fanani walikuwa bibi na shangazi wa mwali, katika kipindi hicho mafunzo hayo yalimfundisha mwali namna ya kuishi na jamii inayomzunguka na mafunzo yote yalifikishwa kwa njia ya misemo, nyimbo na hadithi. Mfano wa nyimbo zilizokuwa zikiimbwa wakati wa mafunzo hayo ni kama vile:
                                         “Wamala yashi ingano
                                           yaleta bana yao
                                           yenye ubaba ni mama
                                           bayinzilile mwigomba”.
Wimbo huu ulimfundisha mwali kutokumaliza chakula ndani kwa ajili ya matumizi ya baadaye na kwa ajili ya wageni. Pia katika kabila la Wanyakyusa lililopo mkoani Mbeya wilaya za Rungwe, Busokelo na Kyela, mabinti walipewa mafunzo na shangazi pamoja na bibi. Shangazi na bibi waliwafunza mabinti zao namna ya kupika chakula cha kutosha familia, kumtunza mwanaume, kuheshimu wakwe na jamii nzima, kufanya kazi na kulea  watoto vizuri. Ndani ya mafunzo haya, shangazi na bibi walikuwa fanani, binti alikuwa ndiye hadhira na ukweni ndio mahali. Wanyakyusa waliweza kuimba wimbo ufuatao:
                                                Mwanetu                                                                                                                                              ukulile                                                                                                                                                  Bhombaga imbobo                                                                                                                                kundumegho
Tafsiri yake                                                                
                                                 Mtoto wetu                                                                                                                                         umekua                                                                                                                                                fanya kazi                                                                                                                                            kwa mumeo 
Kabla ya utandawazi, fasihi simulizi katika jamii ya Kinyakyusa na Kisafwa zilifunza mabinti na kusaidia maisha yao ya ndoa kuwa salama, tofauti na wakati huu wa Harusi na Kitchen Party (sherehe za kumuaga binti anaeolewa) ambapo vijana hawapewi elimu ya kutosha.                                                              
            Kuonya na kukosoa jamii, zipo tanzu na vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo hujihusisha zaidi na kuiweka jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano; kimaadili kuna methali zinazoonesha maadili mema katika jamii mfano; “Samaki mkunje angali mbichi”, “Mkaidi hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi zipo methali ambazo huonya na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”,Fanya  kazi kama mtumwa uishi kama mfalme”. Pia kupitia hadithi mbalimbali ambazo husimulia zimekuwa ni msaada mkubwa kwa jamii, kwani zimekuwa zikionya na kukosoa jamii, kwa mfano, kabila la wanyakyusa walikuwa wakisimulia hadithi ifuatayo kwa lengo la kuonya na kukosoa watu ambao walikuwa hawataki kusikia ushauri wa wazazi.
                                                    Kapango kapango:
Ijolo alipo bhabha jumo alinumwana unyambala bho akulile kafikile  akabhalilo ka kwegha, bhabha ghwake alimbulile ukuti atikulondighwa ukwegha kutali,(ikikolokyapanja)ghwegheghe unyakyusa,lelo umwene akanile ukwegha unyakyusa abhukile ikikolo kyapanja, bhoafikile munjila alimwaghile undindwana jumo bhalina mama ghwake pasi pa mpiki pakaja pa myabho.Alinganile nukulonda ukumwegha,bho alalusisye ifyuma, mama jula atile ungasosya ifyuma nafimo loli kumpimba mpaka kumyenu. Loli bhobhafikile munjila undindwana jula akanile ukusuluka alyandile ukwimba”
             “ Ghwali nyeghile kumyitu x2
              ikisu kya kutukuju kumyetu kula kula x2”
Pitasi unyambala jula alambalele nu ndindwana jula pa nyuma ngimba akalimundu lyali setano. Lyali ngoghile nukwega indumbula jake, undumyana jula alinkwenda nu kufwa.

Tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili;
                                                               Hadith hadithi:
Hapo zamani za kale palikuwepo na baba mmoja aliyekuwa na mtoto wa kiume. Alipofikia umri wa kuoa baba yake alimwonya kuwa sheria ya Kinyakyusa hairuhusu kuoa nje ya kabila lao lakini yeye alikataa akaondoka kwenda nje ya kabila lake. Alipofika njiani alimkuta binti mmoja na mama yake wakiwa chini ya mti nyumbani kwao. Akampenda yule binti na kuridhia kumuoa. Alipouliza kuhusu mahari yule mama akasema asitoe kitu chochote ila kumbeba hadi nyumbani kwake. Lakini walipofika nyumbani yule binti alikataa kushuka na kuanza kuimba.
      “ulinitoa kwetu x2
        Kaniweke kwangu mji wa Tukuyu, kule kwetu kule x2
Kijana yule baadaye aliamua kulala huku binti akiwa mgongoni. Kumbe hakuwa binti bali ni jini likamuua kwa kumtoa utumbo na ikawa mwisho wa maisha ya yule kijana.

Pia kabila la Wakinga, nao walikuwa na wimbo ambao ulikuwa unatoa maonyo na kukosoa watu wanaotenda matendo ambayo ni kinyume na sheria na kanuni za jamii.

                                    Okhiweni ulukhi pakhiholo ove jova X2                                                                                            wita livava lyong’a ove jova khombe,                                                                                                 witaka omwana we jova X 2
Tafsiri yake
                                    Umeona nini mtoni wewe mama X 2                                                                                                  Unasema unaumwa kiungolila kumbe                                                                                                Unatupa mtoto we mama X 2
Wimbo huu unawaonya na kuwaasa wanawake na wasichana kuwa wasitoe mimba wala kutupa watoto kwani mtoto ni hazina na msaada siku za mbeleni kwani hujui ukizeeka nani atakusaidia (atakayekuzika).                                                                                                                                              Kuchambua na kuchochea umma, kuwafumbua macho, kufichua uozo au uchafu uliomo katika jamii, wasanii wa fasihi simulizi hutunga kazi zao ambazo huwafumbua macho watu kwa kufichuo uozo na maovu yaliyoka katika jamii, kama vile uongozi mbaya, umbea, usaliti, unafiki, wizi, uongo, mila potofu na unyanyasaji wa kijinsia. Kwa mfano, wapo wasani mbalimbali ambao huimba nyimbo ambazo huchambua na kuchochea umma, kuwafumbua macho, kufichuo uozo na uchafu uliomo katika jamii, baadhi ya wasanii hao ni kama Mrisho Mpoto wimbo wake wa Chochea kuni na Mjomba ni nyimbo ambazo zimebeba maudhui ya kufichuo uozo uliomo katika jamii kama vile uongozi mbaya, usaliti, matabaka, hali ngumu ya maisha ya watanzania na unyonyaji. Pia, msanii Roma ana nyimbo ambazo hufumbua macho jamii, nyimbo hizo ni kama Mr. President, Tanzania, Viva Roma hizi ni nyimbo ambazo zimechochea umma wa watanzania na kuwafumbua macho juu ya mwenendo wa siasa na maisha, uongozi mbaya na usaliti. Pia msanii kutoka Afrika Kusini marehem Luck Dube kupitia nyimbo zake za Together as one na Different colours ziliwafumbua macho Waafrika kuungana ili kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni, na pia nyimbo zake zilikuwa na maudhui ya kupinga ubaguzi wa rangi.                                                                                                                              Huleta ufahamu juu ya amali na utamaduni wa jamii husika. Fasihi simulizi ya Kiafrika hupelekea kuleta ufahamu juu ya amali za jamii husika, mila na desturi, tamaduni, maadili na hekima ndani ya jamii. Kutokana na fasihi simulizi ya watu wa jamii fulani huishi kwa kufuata miiko, mila na desturi za mahali hapo. Kutokana na tamaduni hizo kunakuwa na amali ya kutosha inayowafanya watu hao waishi kwa furaha na kufanya shughuli zao za kimaendeleo. Kwa mfano, katika jamii ya Wanyakyusa mabinti waliweza kuishi kwa kujitunza ili waweza kutunza mila na desturi za Kinyakyusa, mabinti waliishi kimaadili bila kuingiliwa kimwili yaani wasipoteze “ubikra wao” kwa binti aliyepoteza ubikra aliitwa “bhalile inguku” yaani “hamna au wamekula wakuku” wakiwa na maana “hana bikra”. Binti huyo alitolewa mali chache (ng’ombe) na kuonekana hafai katika jamii, pia amewadhalilisha wazazi wake. Hivyo mabinti waliishi kwa kuogopa kuingia katika mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo ama kabla hajaolewa. Binti aliyeolewa akiwa na bikra alitolewa mali nyingi na alileta heshima kubwa kwa wazazi wake. Pia kuna nahau mbalimbali za Kiswahili ambazo hutumika kutoa maadili na kuonesha utamaduni wa jamii husika mfano:
                                                Achiwa mkopa                                                                                                                                                maana yake: Rithishwa kazi ya uganga          
                                                Chinja kafara                                                                                                                                      maana yake: toa sadaka                     
Nahau hizi zilitumika sana katika jamii nyingi za Waswahili, kwa lengo la kutoa maadili na kuendeleza amali na utamaduni wa jamii.                                                                                        Kuhimiza kazi: Fasihi simulizi ya Kiafrika ilihimiza sana kazi na hii elimu ilitolewa wakati wa jando na unyango.  Jando na unyago ni sehemu ya malezi yanayolenga kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake ya kuwa mwanaume au mwanamke ili jinsia imjenge badala ya kumvuruga. Mara nyingi wavulana huwa wanaongelea siri zao zinazowahusu wao katika makuzi yao na huwa hawataki mtoto wa kike kuzijua hali kadhalika kwa upande wa mtoto wa kike nao huwa wana mafunzo yao ambapo nao huwa hawapendi mambo wanayojifunza yajulikane kwa watoto wa kiume, mafunzo haya yaliweza kutolewa na watu wazima ambao ndio walitegemewa zaidi na jamii katika kutoa elimu ya jinsia. Katika jamii za kibantu zilikuwa na kawaida ya kuongelea mafunzo hayo ya siri na wazee hasa babu na bibi ndio walihusika sana katika kutoa mafunzo hayo, kulikuwa na mafundisho rasmi ambayo yalikuwa na umuhimu wa kujua mapema ukweli hasa kuhusu maumbile ya binadamu. Kadri mtoto anavyozidi kukua ndivyo alivyohitaji kujifahamu kijinsia ili aweze kukomaa na hatimaye kukabiliana na shughuli mbalimbali za kijamii. Kwa  mfano, Katika kabila la Wanyakyusa walizingatia malezi ya vijana na ilikuwa ni mwiko kwa mtoto wa kinyakyusa kudeka, mama aliweza kula na watoto wa kiume chini ya miaka kumi pamoja na wale wa kike ambao walikuwa bado hawajaolewa, lengo kubwa ilikuwa ni kuwafundisha kula kwa adabu na kuheshimiana. Kwa upande wa mtoto wa kiume aliruhusiwa kukaa na mama yake akiwa na umri chini ya miaka kumi, baada ya umri huo hakuruhusiwa kukaa tena na mama yake bali aliambatana na wanaume kwa lengo la kujifunza kazi. Mgawanyo wa kazi ulizingatia umri na jinsi kwa kuwa zamani watoto wengi hawakuwa na fursa za kusoma, hivyo walipata elimu (mafunzo) kutoka kwa wazazi wao. Watoto walipofikisha umri wa miaka kumi na moja au kumi na mbili waliweza kukusanywa kutoka familia tofauti na kupelekwa mbali na wazazi wao ili kujifunza maisha na kujitegemea na hivyo kuweza kuanzisha vijiji vipya kwa kujenga nyumba kisha kuanzisha familia.
Wakati wa utoaji wa mafunzo hayo semi na nyimbo mbalimbali zilitumika na zilitolewa na wazee, kwa mfano:
                                           “ Ukukoma ingunguni”
             Tafsiri yake ni;        “Kuua kunguni” 
Msemo huu ulilenga kuelimisha watoto na kuwakomaza kuwa kuendelea kuishi kwenye nyumba ya wazazi pamoja nao na hali wakiwa wamefikia umri wa kujitegemea sio vizuri, hivyo walisisitizwa zaidi kujitegemea. (Mwambusye, 2012:23).
                                              “Ukukula kitalikitali
             Tafsiri yake ni;     “Kukua haraharaka lakini bila umbile na akili au hekima”.
Katika msemo huu walimaanisha zaidi kuwa mwili unakua upesi kuliko akili yaani ukuaji wa mwili hauendi sambamba na ukuaji wa akili (Mwambusye, 2012:27).
Kutokana na mafunzo haya ya kukaa pamoja, vijana waliweza kujifunza majukumu mbalimbali na malezi ya jamii zao kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na kuhimiza ushirikiano, kuheshimiana na kuthaminiana na hatimiye kuishi kama ndugu na jamii moja na hapo ndipo  Wanyakyusa wanapo sema:
                                            “Nkamu ju mundu
                 Tafsiri yake ni:   “Undugu ni kufaana na sio kufanana”.
Pia kuna methali ya Kiswahili inayosema Mgagaa na upwa hali wali mkavu, methali hii inahimiza wanajamii kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi mahitaji yao. Hivi ndivyo fasihi simulizi ya kiafrika ilivyokuwa ikihimiza masuala ya kazi, kufanya kazi kwa bidiii.                                                          Kuipa jamii mwelekeo. Kwa kuelimisha na kuyapitisha mawazo yanayohusiana na jamii fulani, wanajamii wanahakikisha kuwa jamii imepata mwelekeo. Katika vitanzu vya fasihi simulizi huwako na adili na ujumbe ambao unawaelekeza, kuwaadibu, kuwaonya na kuwaongoza kwenye matarajio mema ya jamii husika. Kwa mfano, katika jamii nyingi, fasihi simulizi ilitumiwa kama njia ya kuwaelekeza na kuwafundisha vijana mwenendo mzuri, maadili yafaayo pamoja na falsafa ifaayo katika jamii. Kwa mfano, jamii ya Waswahili, Unguja na Pemba huimba sana wimbo ufuatao lengo lilikuwa kuwatia moyo vijana.
                                    Mwanangu amba duni hino,                                                                                                               Ndo urume                                                                                                                                          Mrume hujikaza mrume                                                                                                                       Mrume mwana hujikaza mrume
                                   
Mume wangu mwanao alia                                                                                         Memeze ngariba kamchachia

Mwanangu ukubwa una raha                                                                                     Hili shida uje uone                                                                                                           Mwanangu shika mndu na msaha                                                                          Uchimbe shimo wasivione                                                                                          Ruka ukijitoa tunawe                                                                                                   Mwana wa hali ni watu wenyewe

            Kuhimiza umoja na mshikamano, fasihi simulizi ya kiafrika huhimiza jamii kuwa na mshikamano ili kuleta maendeleo katika jamii zao. Kwa mfano methali ya Kiswahili inayosema kidole kimoja hakivunji chawa, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Methali hizi husisitiza suala la umoja na mshikamo miongoni mwa wanajamii. Pia, Katika kabila la Wanyakyusa na Wasafwa wana namna moja katika kushirikiana wakati wa misiba na matatizo mbalimbali kwa mfano, ukitokea msiba katika familia fulani kwenye jamii, jamii nzima huhusika katika msiba ule na kushirikiana katika shughuli zote za msiba huo. Wanaume na wanawake wa jamii nzima waliwajibika kushinda na kulala mahali palipotokea msiba na kila mmoja katika jamii huweza kuchangia chakula, kuni na vifaa vingine vilivyotumika katika shughuli nzima ya mazishi kama vile majembe, makoleo, mkeka na ng’ombe, hii ilikuwa ni kulingana na uzito wa msiba uliokuwa umetokea. Mbolezi ziliimbwa wakati wote wa msiba ambapo waghani walikuwa wakitaja sifa na mema ya marehemu au ukoo wa marehemu, waombolezaji wengine waliimba na kupita sehemu mbalimbali za makazi yao wakiimba na kuchangishana nafaka kwa ajili ya msiba, kwa mfano katika kabila la Wasafwa walikuwa wanaimba nyimbo kama hizi:
                                       “Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile      
                                        Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile
                                        Kiongozi:     (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile”.
Tafsiri yake
                                    Kiongozi: Ndio maana x 2                                                                                                                Waitikaji: Ndio maana tumekuja                                                                                                        Kiongozi: Ndio maana x 2                                                                                                                       Waitikiaji: Ndio maana tumekuja                                                                                                          Kiongozi: (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)                                                                              Waitikiaji: Ndio maana tumekuja”.

Wimbo huu hutumika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya jamii na ndugu pamoja na jamaa waliofiwa, wimbo una maana kuwa (Tumekuja kwa sababu tunaushirikiano na nyie).
Kwa upande wa kabila la Wanyakyusa waliimba hivi:
                                       “Kiongozi:   Twalimenye naloli           
                                        Waitikiaji:  Twalimenye naloli
                                         Kiongozi:   Ukete abhandu bikulila
                                         Waitikiaji: Ukete abhandu bikulila
                                         Kiongozi:  Keta tukwenda tukulila
                                         Waitikiaji: Keta tukwenda tukulila”
Tafsiri yake:
                                       “Kiongozi:  Tulimjua sana       
                                        Waitikiaji: Tulimjua sana
                                        Kiongozi:   Ona watu wanavyolia
                                        Waitikiaji:  Ona watu wanavyolia
                                        Kiongozi:   Tazama tunatembea tukilia
                                        Waitikiaji:  Tazama tunatembea tukilia”.

Nyimbo hizi ni za maombolezo na zilikuwa zikiimbwa wakati wa msiba, wanajamii waliimba kwa lengo la kumkubuka marehemu au ndugu yao aliyewatoka.                                                    Kwa ujumla, fasihi simulizi ni zao la jamii na inafungamana na maisha ya watu. Fasihi simulizi inazungumzia juu ya mwanadamu na mazingira yake. Kukua kwa sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha utandawazi. Kutokana na mabadiliko haya, fasihi simulizi kama kazi ya kisanaa iliyojaa ufundi na ubunifu ndani yake haina budi kuendana na mabadiliko hayo maana hata mfumo wa maisha hubadilikabadilika katika jamii kulingana na maendeleo yanavyozidi kuimarika na kujitokeza. Hivyo pamoja na mabadiliko hayo si vyema kupuuza fasihi simulizi kwani yenyewe ndiyo fasihi kongwe na ndiyo iliyoibua fasihi andishi baada ya kugundulika kwa maandishi kwani fasihi hata kabla ya utandawazi ilikuwa na mchango mkubwa sana katika kuimarisha na kutoa elimu kwa jamii.


                                     





                                          MAREJEO

Msokile, M. (1992). Misingi ya Hadithi Fupi. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.

Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Syambo, B. na Mazrui, A. (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: EAEP.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI.

Wamitila, K.W (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi.Nairobi: Focus Publications Ltd.
Wamitila, K.W. (2002). Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maoni 4 :

  1. Kazi nzur saana!! Japo kuna swali hapa linasema,jadili jinsi wanaubadilikaji wameathiri waandishi na wahakiki wa kaz za fasihi ya kiswahili

    JibuFuta
  2. Kazi nzuri sana hii, yenye ujazo wa kutosha sanaa!!

    JibuFuta