SWALI: Fasihi simulizi ya Kiafrika ni mfumo
kamili wa elimu ya maisha ya watu. Kwa kutumia mifano, kutoka fasihi simulizi
za jamii mbalimbali za Kitanzania. Jadili rai hii.
Dhana ya fasihi simulizi imeweza
kutolewa fasili mbalimbali na wataalamu na wanazuoni mbalimbali, kutoka maeneo
tofautitofauti. Fasili hizi mbalimbali zilizotolewa na wanazuoni na wataalamu
wengi zimetokana na tofauti miongoni mwao katika mitazamo ya chimbuko la fasihi
simulizi, kinadharia na matumizi ya fasihi simulizi kati ya jamii moja na
nyingine kumepelekea kuwepo kwa fasili mbalimbali za fasihi simulizi kama
ifuatavyo
Mattelu, M.L., (1983:27)
anafafanua kuwa fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika
kuumba, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
Anaendelea kusema kuwa fasihi simulizi ikiwa ni sanaa itumiayo maneno katika
kutoa dhana fulani, hutegemea sana nyenzo mbalimbali za kuonekana na kusikika
zitumiwazo na binadamu katika kujieleza.
Msokile, M (1992:3)
fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha, kazi hii ya sanaa
huhifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Mwisho
anaeleza kuwa fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Maelezo
haya ya Msokile yanashabihiana na TUKI (2004) fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi
inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya
mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Mazrui na Syambo (1992)
wanasema fasihi simulizi ni sanaa ya matumizi ya lugha ya kubuni inayosambazwa
kwa mdomo, kwa njia ya kuimba, kuchezwa, kuigizwa, kusimuliwa, kuumba, kufumbua
au kutegua mafumbo ya vitendawili. Pia
naye Mulokozi, M.M (1996) anasema, fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au
kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila
kutumia maandishi. Baada ya kuangalia maoni
mbalimbali ya wataalamu hao, tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa fasihi
simulizi ni aina ya fasihi inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya masimulizi
ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi, na hurithishwa kutoka kizazi kimoja
hadi kingine. Fasihi
simulizi ya Kiafrika ni ile fasihi ambayo kwa asili yake imechimbuka na kuibuliwa
na Waafrika wenyewe na huwasilishwa kwa njia ya mdomo kwa kusimuliwa, kuimbwa,
kutongolewa au kughaniwa. Fasihi hii ina mawanda mapana kwani hujumuisha jamii
zote za Kiafrika na makabila yote ya Kiafrika kama vile Wabuganda kutoka nchini
Kenya, Wazulu kutoka Afrika Kusini, Kikuyu kutoka nchini Kenya, Wakinga,
Wabena, Wapare, Wasukuma kutoka nchini Tanzania. Pia
fasihi hii hujumuisha lugha mbalimbali za kiafrika, tamaduni zao, nyimbo zao,
mila na desturi zao kama vile matambiko , jando na unyango, kwa mfano kabila la
Wakinga linalopatikana mkoani Njombe nchini Tanzania wanamsitu wao ambao watu
wa kabila hili huenda kuomba kutatuliwa matatizo yao, shida na shukurani kwa
mungu wao, msitu huo unaitwa Nyumba nitu. Ni
kweli kabisa fasihi simulizi ya kiafrika ni mfumo wa elimu ya maisha ya watu.
Kauli hii inaweza kufafanuliwa zaidi kwamba, ndani ya fasihi simulizi ambapo
kuna tanzu na vipera mbalimbali vinavyotendwa na wasanii katika jamii huchochea
na kuhamasisha ujifunzaji, uelewaji na kuongeza maarifa katika mfumo mzima wa
maisha ya mtu au jamii. Kupitia vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi kama
vile nahau, nyimbo, vitendawili, soga, ngano, tendi, mashairi, majigambo,
ngonjera, visasili, na tarihi, vimekuwa kama darasa katika kuleta elimu ya
maisha ya watu ndani ya jamii katika kuendesha maisha yao. Fasihi simulizi huendana
na muktadha katika utendaji wake, kama asemavyo Mulokozi, M.M. (1996: 24) kuwa
fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha fulani wa jamii na
kutawaliwa na mwingiliano wa fanani, hadhira, fani inayotendwa, tukio, mahali
na wakati.
Hivyo basi, fasihi
simulizi ya kiafrika ni mfumo kamili wa elimu ya watu katika muktadha fulani
katika jamii fulani, katika shughuli zao za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na
kijamii kwa sababu zifuatazo:
Kufunza jamii: Fasihi
simulizi ya Kiafrika hupelekea mafunzo juu ya maisha ya ndoa. Katika kipengele
hiki, vijana waliweza kupata mafunzo ya ndoa kabla ya kuanza maisha ya ndoa.
Kwa mfano, Suala la ndoa katika
kabila la wasafwa wanaopatikana wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya waliohusika
kumfundisha mwali ni shangazi na bibi ambao hasa walikuwa ndio fanani, mwali
huyo alifundishwa namna ya kuishi katika ndoa pamoja na matumizi mazuri ya
chakula katika familia, kwa mfano binti alifundishwa kupika chakula ambacho
kingetosheleza mahitaji ya mumewe na familia yake kwa ujumla bila kubakiza na
kukitupa. Katika shughuli hii mwali ndiye aliyekuwa hadhira na ukweni ndio
palikuwa mahali pa kutendea na maudhui yalikuwa ni mafunzo kuhusu maisha ya
ndoa na fanani walikuwa bibi na shangazi wa mwali, katika kipindi hicho mafunzo
hayo yalimfundisha mwali namna ya kuishi na jamii inayomzunguka na mafunzo yote
yalifikishwa kwa njia ya misemo, nyimbo na hadithi. Mfano wa nyimbo zilizokuwa
zikiimbwa wakati wa mafunzo hayo ni kama vile:
“Wamala yashi ingano
yaleta bana yao
yenye
ubaba ni mama
bayinzilile mwigomba”.
Wimbo
huu ulimfundisha mwali kutokumaliza chakula ndani kwa ajili ya matumizi ya
baadaye na kwa ajili ya wageni. Pia katika kabila la Wanyakyusa lililopo mkoani
Mbeya wilaya za Rungwe, Busokelo na Kyela, mabinti walipewa mafunzo na shangazi
pamoja na bibi. Shangazi na bibi waliwafunza mabinti zao namna ya kupika chakula
cha kutosha familia, kumtunza mwanaume, kuheshimu wakwe na jamii nzima, kufanya
kazi na kulea watoto vizuri. Ndani ya
mafunzo haya, shangazi na bibi walikuwa fanani, binti alikuwa ndiye hadhira na
ukweni ndio mahali. Wanyakyusa waliweza kuimba wimbo ufuatao:
“Mwanetu ukulile Bhombaga imbobo kundumegho”
Tafsiri yake
“ Mtoto
wetu umekua fanya kazi
kwa mumeo”
Kabla
ya utandawazi, fasihi simulizi katika jamii ya Kinyakyusa na Kisafwa zilifunza
mabinti na kusaidia maisha yao ya ndoa kuwa salama, tofauti na wakati huu wa
Harusi na Kitchen Party (sherehe za kumuaga binti anaeolewa) ambapo vijana
hawapewi elimu ya kutosha.
Kuonya na kukosoa jamii, zipo tanzu na
vipera mbalimbali vya fasihi simulizi ambavyo hujihusisha zaidi na kuiweka
jamii katika nafasi iliyobora zaidi. Mfano; kimaadili kuna methali zinazoonesha
maadili mema katika jamii mfano; “Samaki
mkunje angali mbichi”, “Mkaidi
hafaidi mpaka siku ya iddi”. Vilevile kiuchumi zipo methali ambazo huonya
na kukosoa wale wote wenye tabia za kivivu katika kujitafutia maisha mfano, “Mtegemea cha ndugu hufa masikini”, “Fanya
kazi kama mtumwa uishi kama mfalme”. Pia kupitia hadithi mbalimbali
ambazo husimulia zimekuwa ni msaada mkubwa kwa jamii, kwani zimekuwa zikionya
na kukosoa jamii, kwa mfano, kabila la wanyakyusa walikuwa wakisimulia hadithi
ifuatayo kwa lengo la kuonya na kukosoa watu ambao walikuwa hawataki kusikia
ushauri wa wazazi.
Kapango kapango:
Ijolo alipo bhabha
jumo alinumwana unyambala bho akulile kafikile akabhalilo ka kwegha,
bhabha ghwake alimbulile ukuti atikulondighwa ukwegha
kutali,(ikikolokyapanja)ghwegheghe unyakyusa,lelo umwene akanile ukwegha
unyakyusa abhukile ikikolo kyapanja, bhoafikile munjila alimwaghile undindwana
jumo bhalina mama ghwake pasi pa mpiki pakaja pa myabho.Alinganile nukulonda
ukumwegha,bho alalusisye ifyuma, mama jula atile ungasosya ifyuma nafimo loli
kumpimba mpaka kumyenu. Loli bhobhafikile munjila undindwana jula akanile
ukusuluka alyandile ukwimba”
“ Ghwali nyeghile kumyitu x2
ikisu kya kutukuju kumyetu kula kula x2”
Pitasi unyambala jula alambalele nu ndindwana jula pa nyuma ngimba
akalimundu lyali setano. Lyali ngoghile nukwega indumbula jake, undumyana jula
alinkwenda nu kufwa.
Tafsiri yake kwa
lugha ya Kiswahili;
Hadith hadithi:
Hapo zamani za kale
palikuwepo na baba mmoja aliyekuwa na mtoto wa kiume. Alipofikia umri wa kuoa
baba yake alimwonya kuwa sheria ya Kinyakyusa hairuhusu kuoa nje ya kabila lao
lakini yeye alikataa akaondoka kwenda nje ya kabila lake. Alipofika njiani alimkuta
binti mmoja na mama yake wakiwa chini ya mti nyumbani kwao. Akampenda yule
binti na kuridhia kumuoa. Alipouliza kuhusu mahari yule mama akasema asitoe
kitu chochote ila kumbeba hadi nyumbani kwake. Lakini walipofika nyumbani yule
binti alikataa kushuka na kuanza kuimba.
“ulinitoa kwetu x2
Kaniweke kwangu mji wa Tukuyu, kule kwetu kule x2
Kijana yule baadaye
aliamua kulala huku binti akiwa mgongoni. Kumbe hakuwa binti bali ni jini
likamuua kwa kumtoa utumbo na ikawa mwisho wa maisha ya yule kijana.
Pia kabila la Wakinga, nao walikuwa na wimbo ambao ulikuwa unatoa
maonyo na kukosoa watu wanaotenda matendo ambayo ni kinyume na sheria na kanuni
za jamii.
“Okhiweni
ulukhi pakhiholo ove jova X2 wita livava lyong’a ove jova khombe, witaka omwana we jova X 2
Tafsiri yake
Umeona
nini mtoni wewe mama X 2 Unasema unaumwa kiungolila kumbe Unatupa
mtoto we mama X 2
Wimbo huu
unawaonya na kuwaasa wanawake na wasichana kuwa wasitoe mimba wala kutupa
watoto kwani mtoto ni hazina na msaada siku za mbeleni kwani hujui ukizeeka
nani atakusaidia (atakayekuzika). Kuchambua
na kuchochea umma, kuwafumbua macho, kufichua uozo au uchafu uliomo katika
jamii, wasanii wa fasihi simulizi hutunga kazi zao ambazo huwafumbua macho watu
kwa kufichuo uozo na maovu yaliyoka katika jamii, kama vile uongozi mbaya,
umbea, usaliti, unafiki, wizi, uongo, mila potofu na unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa mfano, wapo wasani mbalimbali ambao huimba nyimbo ambazo huchambua na kuchochea
umma, kuwafumbua macho, kufichuo uozo na uchafu uliomo katika jamii, baadhi ya
wasanii hao ni kama Mrisho Mpoto wimbo wake wa Chochea kuni na Mjomba
ni nyimbo ambazo zimebeba maudhui ya kufichuo uozo uliomo katika jamii kama
vile uongozi mbaya, usaliti, matabaka, hali ngumu ya maisha ya watanzania na
unyonyaji. Pia, msanii Roma ana nyimbo ambazo hufumbua macho jamii, nyimbo hizo
ni kama Mr. President, Tanzania, Viva Roma
hizi ni nyimbo ambazo zimechochea umma wa watanzania na kuwafumbua macho juu ya
mwenendo wa siasa na maisha, uongozi mbaya na usaliti. Pia msanii kutoka Afrika
Kusini marehem Luck Dube kupitia nyimbo zake za Together as one
na Different colours ziliwafumbua macho Waafrika kuungana ili
kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni, na pia nyimbo zake zilikuwa na maudhui
ya kupinga ubaguzi wa rangi. Huleta
ufahamu juu ya amali na utamaduni wa jamii husika. Fasihi simulizi ya Kiafrika hupelekea
kuleta ufahamu juu ya amali za jamii husika, mila na desturi, tamaduni, maadili
na hekima ndani ya jamii. Kutokana na fasihi simulizi ya watu wa jamii fulani
huishi kwa kufuata miiko, mila na desturi za mahali hapo. Kutokana na tamaduni
hizo kunakuwa na amali ya kutosha inayowafanya watu hao waishi kwa furaha na
kufanya shughuli zao za kimaendeleo. Kwa mfano, katika jamii ya Wanyakyusa
mabinti waliweza kuishi kwa kujitunza ili waweza kutunza mila na desturi za
Kinyakyusa, mabinti waliishi kimaadili bila kuingiliwa kimwili yaani wasipoteze
“ubikra wao” kwa binti aliyepoteza ubikra aliitwa “bhalile inguku” yaani “hamna
au wamekula wakuku” wakiwa na maana “hana bikra”. Binti huyo alitolewa mali
chache (ng’ombe) na kuonekana hafai katika jamii, pia amewadhalilisha wazazi
wake. Hivyo mabinti waliishi kwa kuogopa kuingia katika mahusiano ya kimapenzi
katika umri mdogo ama kabla hajaolewa. Binti aliyeolewa akiwa na bikra alitolewa
mali nyingi na alileta heshima kubwa kwa wazazi wake. Pia kuna nahau mbalimbali
za Kiswahili ambazo hutumika kutoa maadili na kuonesha utamaduni wa jamii
husika mfano:
Achiwa
mkopa maana yake: Rithishwa kazi ya
uganga
Chinja
kafara maana yake: toa
sadaka
Nahau hizi
zilitumika sana katika jamii nyingi za Waswahili, kwa lengo la kutoa maadili na
kuendeleza amali na utamaduni wa jamii. Kuhimiza
kazi: Fasihi simulizi ya Kiafrika ilihimiza sana kazi na hii elimu ilitolewa
wakati wa jando na unyango. Jando na unyago ni sehemu ya malezi yanayolenga
kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake ya kuwa mwanaume au mwanamke ili jinsia
imjenge badala ya kumvuruga. Mara nyingi wavulana huwa wanaongelea siri zao
zinazowahusu wao katika makuzi yao na huwa hawataki mtoto wa kike kuzijua hali
kadhalika kwa upande wa mtoto wa kike nao huwa wana mafunzo yao ambapo nao huwa
hawapendi mambo wanayojifunza yajulikane kwa watoto wa kiume, mafunzo haya
yaliweza kutolewa na watu wazima ambao ndio walitegemewa zaidi na jamii katika
kutoa elimu ya jinsia. Katika jamii za kibantu zilikuwa na kawaida ya kuongelea
mafunzo hayo ya siri na wazee hasa babu na bibi ndio walihusika sana katika
kutoa mafunzo hayo, kulikuwa na mafundisho rasmi ambayo yalikuwa na umuhimu wa
kujua mapema ukweli hasa kuhusu maumbile ya binadamu. Kadri mtoto anavyozidi kukua
ndivyo alivyohitaji kujifahamu kijinsia ili aweze kukomaa na hatimaye
kukabiliana na shughuli mbalimbali za kijamii. Kwa mfano, Katika kabila la Wanyakyusa
walizingatia malezi ya vijana na ilikuwa ni mwiko kwa mtoto wa kinyakyusa
kudeka, mama aliweza kula na watoto wa kiume chini ya miaka kumi pamoja na wale
wa kike ambao walikuwa bado hawajaolewa, lengo kubwa ilikuwa ni kuwafundisha
kula kwa adabu na kuheshimiana. Kwa upande wa mtoto wa kiume aliruhusiwa kukaa
na mama yake akiwa na umri chini ya miaka kumi, baada ya umri huo hakuruhusiwa
kukaa tena na mama yake bali aliambatana na wanaume kwa lengo la kujifunza
kazi. Mgawanyo wa kazi ulizingatia umri na jinsi kwa kuwa zamani watoto wengi
hawakuwa na fursa za kusoma, hivyo walipata elimu (mafunzo) kutoka kwa wazazi
wao. Watoto walipofikisha umri wa miaka kumi na moja au kumi na mbili waliweza
kukusanywa kutoka familia tofauti na kupelekwa mbali na wazazi wao ili
kujifunza maisha na kujitegemea na hivyo kuweza kuanzisha vijiji vipya kwa
kujenga nyumba kisha kuanzisha familia.
Wakati
wa utoaji wa mafunzo hayo semi na nyimbo mbalimbali zilitumika na zilitolewa na
wazee, kwa mfano:
“ Ukukoma ingunguni”
Tafsiri yake
ni; “Kuua kunguni”
Msemo
huu ulilenga kuelimisha watoto na kuwakomaza kuwa kuendelea kuishi kwenye
nyumba ya wazazi pamoja nao na hali wakiwa wamefikia umri wa kujitegemea sio
vizuri, hivyo walisisitizwa zaidi kujitegemea. (Mwambusye, 2012:23).
“Ukukula kitalikitali”
Tafsiri yake ni; “Kukua haraharaka lakini bila umbile na akili
au hekima”.
Katika
msemo huu walimaanisha zaidi kuwa mwili unakua upesi kuliko akili yaani ukuaji
wa mwili hauendi sambamba na ukuaji wa akili (Mwambusye, 2012:27).
Kutokana
na mafunzo haya ya kukaa pamoja, vijana waliweza kujifunza majukumu mbalimbali
na malezi ya jamii zao kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na kuhimiza
ushirikiano, kuheshimiana na kuthaminiana na hatimiye kuishi kama ndugu na
jamii moja na hapo ndipo Wanyakyusa wanapo sema:
“Nkamu ju mundu”
Tafsiri yake ni: “Undugu ni
kufaana na sio kufanana”.
Pia
kuna methali ya Kiswahili inayosema Mgagaa
na upwa hali wali mkavu, methali hii inahimiza wanajamii kufanya kazi kwa
bidii ili kukidhi mahitaji yao. Hivi ndivyo fasihi simulizi ya kiafrika
ilivyokuwa ikihimiza masuala ya kazi, kufanya kazi kwa bidiii. Kuipa
jamii mwelekeo. Kwa kuelimisha na kuyapitisha mawazo yanayohusiana na jamii
fulani, wanajamii wanahakikisha kuwa jamii imepata mwelekeo. Katika vitanzu vya
fasihi simulizi huwako na adili na ujumbe ambao unawaelekeza, kuwaadibu,
kuwaonya na kuwaongoza kwenye matarajio mema ya jamii husika. Kwa mfano, katika
jamii nyingi, fasihi simulizi ilitumiwa kama njia ya kuwaelekeza na
kuwafundisha vijana mwenendo mzuri, maadili yafaayo pamoja na falsafa ifaayo
katika jamii. Kwa mfano, jamii ya Waswahili, Unguja na Pemba huimba sana wimbo
ufuatao lengo lilikuwa kuwatia moyo vijana.
Mwanangu amba duni hino, Ndo urume Mrume
hujikaza mrume Mrume
mwana hujikaza mrume
Mume
wangu mwanao alia Memeze
ngariba kamchachia
Mwanangu
ukubwa una raha Hili
shida uje uone Mwanangu
shika mndu na msaha Uchimbe
shimo wasivione Ruka
ukijitoa tunawe Mwana wa
hali ni watu wenyewe
Kuhimiza
umoja na mshikamano, fasihi simulizi ya kiafrika huhimiza jamii kuwa na
mshikamano ili kuleta maendeleo katika jamii zao. Kwa mfano methali ya
Kiswahili inayosema kidole kimoja
hakivunji chawa, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Methali hizi
husisitiza suala la umoja na mshikamo miongoni mwa wanajamii. Pia, Katika
kabila la Wanyakyusa na Wasafwa wana namna moja katika kushirikiana wakati wa
misiba na matatizo mbalimbali kwa mfano, ukitokea msiba katika familia fulani
kwenye jamii, jamii nzima huhusika katika msiba ule na kushirikiana katika
shughuli zote za msiba huo. Wanaume na wanawake wa jamii nzima waliwajibika
kushinda na kulala mahali palipotokea msiba na kila mmoja katika jamii huweza
kuchangia chakula, kuni na vifaa vingine vilivyotumika katika shughuli nzima ya
mazishi kama vile majembe, makoleo, mkeka na ng’ombe, hii ilikuwa ni kulingana
na uzito wa msiba uliokuwa umetokea. Mbolezi ziliimbwa wakati wote wa msiba
ambapo waghani walikuwa wakitaja sifa na mema ya marehemu au ukoo wa marehemu,
waombolezaji wengine waliimba na kupita sehemu mbalimbali za makazi yao
wakiimba na kuchangishana nafaka kwa ajili ya msiba, kwa mfano katika kabila la
Wasafwa walikuwa wanaimba nyimbo kama hizi:
“Kiongozi: Ndio
maana ×2
Waitikiaji:
Ndio maana twinzile
Kiongozi: Ndio maana ×2
Waitikiaji: Ndio maana twinzile
Kiongozi: (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
Waitikiaji: Ndio maana twinzile”.
Tafsiri yake
“Kiongozi: Ndio maana x 2 Waitikaji: Ndio maana tumekuja
Kiongozi: Ndio maana x 2
Waitikiaji: Ndio maana tumekuja
Kiongozi: (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
Waitikiaji: Ndio maana tumekuja”.
Wimbo
huu hutumika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya jamii na ndugu pamoja na jamaa
waliofiwa, wimbo una maana kuwa (Tumekuja kwa sababu tunaushirikiano na nyie).
Kwa
upande wa kabila la Wanyakyusa waliimba hivi:
“Kiongozi: Twalimenye
naloli
Waitikiaji: Twalimenye naloli
Kiongozi:
Ukete abhandu bikulila
Waitikiaji: Ukete abhandu bikulila
Kiongozi: Keta tukwenda tukulila
Waitikiaji: Keta tukwenda tukulila”
Tafsiri
yake:
“Kiongozi: Tulimjua
sana
Waitikiaji: Tulimjua sana
Kiongozi: Ona watu wanavyolia
Waitikiaji: Ona watu wanavyolia
Kiongozi: Tazama tunatembea tukilia
Waitikiaji:
Tazama tunatembea tukilia”.
Nyimbo hizi ni za
maombolezo na zilikuwa zikiimbwa wakati wa msiba, wanajamii waliimba kwa lengo
la kumkubuka marehemu au ndugu yao aliyewatoka. Kwa
ujumla, fasihi simulizi ni zao la jamii na inafungamana na maisha ya watu.
Fasihi simulizi inazungumzia juu ya mwanadamu na mazingira yake. Kukua kwa
sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo katika
nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambapo maendeleo ya sayansi na
teknolojia yamesababisha utandawazi. Kutokana na mabadiliko haya, fasihi
simulizi kama kazi ya kisanaa iliyojaa ufundi na ubunifu ndani yake haina budi
kuendana na mabadiliko hayo maana hata mfumo wa maisha hubadilikabadilika
katika jamii kulingana na maendeleo yanavyozidi kuimarika na kujitokeza. Hivyo
pamoja na mabadiliko hayo si vyema kupuuza fasihi simulizi kwani yenyewe ndiyo
fasihi kongwe na ndiyo iliyoibua fasihi andishi baada ya kugundulika kwa maandishi
kwani fasihi hata kabla ya utandawazi ilikuwa na mchango mkubwa sana katika
kuimarisha na kutoa elimu kwa jamii.
MAREJEO
Msokile, M. (1992). Misingi ya
Hadithi Fupi. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Mulokozi,
M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi
Simulizi ya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Syambo, B. na Mazrui, A.
(1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi:
EAEP.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili
Sanifu. Dar es Salaam: TUKI.
Wamitila,
K.W (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi
na Andishi.Nairobi: Focus Publications Ltd.
Wamitila, K.W. (2002). Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele
Vyake. Nairobi: Phoenix Publishers.
Kazi nzur saana!! Japo kuna swali hapa linasema,jadili jinsi wanaubadilikaji wameathiri waandishi na wahakiki wa kaz za fasihi ya kiswahili
JibuFutaMmmmh
JibuFutaKazi nzuri
JibuFutaKazi nzuri sana hii, yenye ujazo wa kutosha sanaa!!
JibuFuta